Waajiri na watendaji wa Kata ,Mitaa na Vijiji wametakiwa kutopokea fedha kwa waombaji wa nafasi ya ukarani katika zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika agosti 23 mwaka huu Nchini kote kwani tabia hiyo haikubaliki.
Rai hiyo imetolewa leo na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022,Mhe. Anna Makinda katika kikao kazi cha Maafisa habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali kinachofanyika mkoani Tanga.
Mhe. Makinda amesema kuwa, wapo baadhi ya waajiri kutaka watumishi wao kutoa fedha ili wapitishe maombi yao sambamba na watendaji kutaka malipo ili kugonga mihuri katika fomu za maombi ya ukarani wa sensa.
Ametoa angalizo kwa wananchi na watumishi wote wenye nia ya kuomba kazi ya ukarani wa sensa kutotoa fedha yoyote ili kupata kazi ya sensa,kwani maombi hayo yanapokelewa kupitia mtandao na sio ana kwa ana, ili kupata watu wenye uwezo na sifa na sio kwa kigezo cha undugu au kufahamiana.
Aidha,amesema kuwa maandalizi ya sensa hadi sasa yamekamilika kwa asilimia 81,hivyo wananchi wajiandae kuhesabiwa ili kupata takwimu sahihi za watu na majengo yaliyopo nchini.
"Sensa ya mwaka huu ina sehemu kuu mbili,sehemu ya Sensa ya watu na sehemu ya Sensa ya majengo, ambayo kwa mara ya kwanza inafanyika nchini mwaka huu ili kutambua idadi ya majengo yaliyopo nchini na matumizi yake ili kuwezesha Serikali katika sera ya ardhi",alisema Makinda.
Nafasi za ukarani wa sensa ni karani wa kuhesabu watu,karani wa usimamizi wa maudhui na karani wasimamizi wa TEHAMA na sifa kuu ya mwombaji wa nafasi hizo ni pamoja na uwezo wa kutumia Simu janja kwani Sensa ya mwaka huu itatumia TEHAMA tofauti na sensa zilizopita.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.