Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Ndugu Sunday Deogratias, ametoa wito kwa watumishi wapya 43 kutoka kada za afya na kilimo walioripoti wilayani humo kuhakikisha wanaangalia maendeleo yao binafsi kwa kufanya kazi kwa bidii na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza katika semina maalum ya kuwakaribisha watumishi hao wapya iliyofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri, Ndugu Deogratias amewataka watumishi hao kuwa na mtazamo chanya wa kujiletea maendeleo kupitia fursa nyingi zinazopatikana wilayani humo.
“Wilaya ya Ludewa imezungukwa na fursa nyingi. Ardhi bado ipo ya kutosha, bei za kununua au kukodi mashamba si kubwa kama ilivyo maeneo mengine. Halmashauri yetu ina kanda tatu zinazofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali – hiyo ni fursa. Fikeni vituoni mkatafakari ni nini mnaweza kufanya zaidi ya kazi ya kila siku,” alisema Mkurugenzi.
Amewahimiza pia kutumia nafasi hiyo kujenga maisha yao mapema kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo kilimo na ufugaji. “Napenda kuwaona mkijenga nyumba nzuri kabla ya kustaafu. Napenda watumishi ambao wamejijenga kiuchumi, manung’uniko hayatakuwepo,” alisisitiza.
Aidha, Mkurugenzi huyo amewakumbusha kuhusu miradi mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kuanza hivi karibuni katika wilaya hiyo, ikiwemo miradi ya Liganga na Mchuchuma, na kueleza kuwa uwekezaji huo utavutia watu wengi hivyo kuongeza mahitaji ya bidhaa na huduma mbalimbali.
“Watu wengi watakuja Ludewa, mahitaji yataongezeka. Hii ni fursa. Nawasihi mjihusishe na kilimo, ufugaji na shughuli nyingine zitakazowawezesha kuimarisha uchumi wenu binafsi. Mtumishi akiwa na uchumi mzuri hata malalamiko yanapungua,” aliongeza.
Watumishi hao wamepokea maelekezo hayo kwa mshikamano na kuahidi kujituma katika kazi na kuzingatia ushauri walioupata ili kuleta tija binafsi na kwa wananchi wa Ludewa kwa ujumla.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.