Na Chrispin Kalinga
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amepongeza juhudi za mdau wa michezo Kuambiana Investment kwa kuanzisha mashindano ya Kuambiana Cup katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ambayo yanasaidia kuibua vipaji, kukuza na kuendeleza
michezo.
Mhe. Pindi Chana ametoa pongezi hizo Julai 18, 2023 katika Uwanja wa Mpira wa miguu Ngelenge kata ya Ruhuhu wilayani Ludewa wakati akifungua mashindano hayo yaliyoandaliwa na mdau wa Michezo Bw. Imani Kuambiana yaliyodhaminiwa na CRDB, ambapo amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kukuza michezo kuanzia ngazi ya kijiji.
"Wizara kwa mwaka huu wa fedha inaanza Ukarabati wa Viwanja kwa majiji Saba ikiwemo Mwanza, Tanga, Arusha na Mbeya , pamoja na Shule mbili katika kila mkoa ambazo idadi yake ni 56, na tayari tumeanza kuboresha Chuo chetu cha Malya ambacho kinazalisha Wataalam wengi zaidi" amesema Mhe. Chana.
Ameongeza kuwa, Sekta ya Utamaduni na Sanaa inasaidia kuunganisha jamii na kutoa fursa ya ajira kwa watanzania, huku akisistiza kuwa, Tamasha la pili la Utamaduni litakalofanyika mwezi ujao Mkoani Njombe, litatoa fursa kwa vikundi vya Utamaduni na Sanaa kuonesha vipaji na kutangaza Mila na desturi za mikoa yao.
Kwa upande wake muandaji wa Mashindano hayo Bw. Imani Kuambiana amesema lengo la mashindano hayo ni kutoa nafasi kwa vijana waliopo wilaya ya Ludewa ili waoneshe uwezo wao ambapo amealika wadau wengine kuja kuona vipaji hivyo na kuviendeleza.
Mashindano hayo yamejumuisha Tarafa tatu za Wilaya Ludewa na Mshindi atapata Kombe na wengine watapata Jezi pamoja na pesa taslim.
Mheshimiwa Waziri aliambatana na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ludewa akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mhe. Victoria Mwanziva, Mbunge wa Jimbo la Ludewa Mhe. Joseph Kamonga, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Stanley Kolimba, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa pamoja na Afisa Michezo kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.