Maafisa watendaji wa kata 8 za Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa wamekabidhiwa pikipiki zilizotolewa na serikali kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi hapa nchini.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi pikipiki hizo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Mhe. Wise Mgina, amesema kuwa pikipiki hizo ni vifaa muhimu kwa Maafisa hao zinazokwenda kumaliza changamoto ya kutembea umbali mrefu kuwafikia wanachi ili kutoa huduma.
Ameweka wazi kuwa, kata hizo 8 ziko maeneo ya pembezoni zikiwa na maeneo makubwa ya kiutendaji hivyo Maafisa hulazimika kutembea muda mrefu kuwafikia wananchi kutoa huduma jambo ambalo linakwenda kumalizika sasa.
Aidha amewataka Maafisa hao kutumia pikipiki hizo kwa ajili ya kazi iliyokusudiwa na serikali ya kuwahudumia wananchi na si vinginevyo huku akiwasisitiza kuzitunza na kuzithamini kwa kutambua kuwa ni mali ya Umma.
"Tunamshukuru Mhe. Rais kwa kuwathamini Maafisa Watendaji wa kata, kwa kuwa wao ndio wanawahudumia wananchi moja kwa moja, Watendaji mnalo deni sasa, mkatumie vifaa hivi kulingana na malengo yaliyokusudiwa na si kwa matumizi binafsi". Amesisitiza Mwenyekiti Wise Mgina.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ludewa, Komredi Stanley Kolimba, ameipongeza serikali kwa kuteketeleza Ilani ya Chama hicho kwa vitendo, kwa kuhakikisha watumishi wanapata vitendea kazi vitakavyorahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo yao.
"Serikali inawategemea, mmepata usafiri, tumieni muda mwingi kutatua kero na changamoto za wananchi kwenye maeneo ya vijiji na vitongoji vyenu kwa wakati, kwa kufanya hivyo, tutafikia malengo ya serikali ambayo ndio maagizo ya Ilani". Mwenyekiti CCM Kolimba
Zoezi hilo la kuwakabidhi pikipiki limeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mhe. Victoria Mwanziva katika viwanja vya ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.
Kwa upande wao Maafisa Watendaji kata, wameipongeza serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuwapatia usafiri, jambo ambalo wamekiri lilikiwa ni changamoto kubwa iliyokwamisha utendaji kazi katika maeneo yao.
"Kupitia pikipiki hizi zinakwenda kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wetu, jambo la kufanya siku nzima sasa tutatumia saa moja, tunamshukuru Mama Samia na tunaahidi kuwahudumia wananchi kwa kasi kubwa sasa". amefafanua Maria Ngatunga Mtendaji wa Kata ya Madope.
Halmashauri ya wilaya ya Ludewa ni miongoni mwa Halmashauri nchini iliyopata pikipiki 8 kati ya pikipiki 916 zilizotolewa na serikali na kuzigawa kwa Maafisa Watendaji wa kata.
#Ludewa ya Utalii, Uchumi wa Chuma na Mkaa ya Mawe kwa Maendeleo Yetu.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.