Wadau wa Lishe Wilayani Ludewa wamekutana katika kikao cha dharula ili kutathmini hali ya Lishe katika Wilaya hiyo. Mratibu wa Lishe Wilayani humo Bi. Neema Noah amesema wamelazimika kukutana kwa dharula licha ya kwamba hivi karibuni walikuwa wamekaa katika kikao cha kawaida cha tathmini ya robo mwaka katika robo ya pili. Kikao hicho kiliongozwa na Bi. Gladness Mwano ambaye ni Afisa Utumishi na Utawala wa Wilaya akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo. akizungumza katika Kikao hicho Bi Mwano amesema kwamba anawashukuru wajumbe wote walioshiriki kikao hicho muhimu kwani ni kwa maendelea ya afya ya Wanaludewa kwa ujumla, hususani katika kuangazia tatizo sugu la udumavu ambalo limekuwa likilalamikiwa na wadau wengi wa maendeleo Wilayani humo ukizingatia ni Wilaya yenye upatikanaji mkubwa wa Chakula katika Mikoa ya Nyanda za juu kusini.
Kikao hicho ambacho pia kimehudhuriwa na Viongozi wengi sana wa Dini na madhehebu kimekuwa chenye ufanisi kwani mchango mkubwa ulitolewa na Wajumbe, hasa viongozi wa Dini ambapo kwa mtazamo wa Wataalam wa Halmashauri walioshiriki kikao hicho, imeleta hamasa sana kwa maana kwamba ujumbe utafika kwa watu wengi zaidi kwa wakati mmoja na muafaka ikizingatiwa viongozi wa Dini wanajukwaa kubwa la kukutana na wananchi. Viongozi wa Dini walioshiriki kikao hicho ni kutoka Kanisa Katoliki,Bakwata, Sheikh wa Wilaya ya Ludewa, Anglikana,KKKT, TAG, EAGT pamoja na Watendaji wa Kata na wadau wa Lishe. Maeneo kadha yaliyoangaziwa katika kikao hicho ni pamoja na hali ya lishe katika mkoa kwa watoto chini ya miaka mitano, utapiamlo na aina za utapiamlo, mathalani udumavu, ukondefu, uzito pungufu na ukosefu wa vitamini na madini mwilini. Pia kikao hiki kiliangazia sababu za udumavu, athari za udumavu kwa watoto na jamii kwa ujumla, haki za mtoto ikiwemo haki ya kuishi, kuendelezwa, kulindwa, haki ya kushirikiswa katika masuala yanayowahusu watoto wenyewe na haki ya kutobaguliwa. Halikadhalika wajumbe wa kikao waliangazia maeneo yanayopaswa kutekelezwa kama wajibu wa wadau mbalimbali katika jamii katika makundi mbalimbali kama vile wajibu wa wazazi katika malezi, wajibu wa viongozi wa dini katika jamii na wajibu wa jamii nzima kwa ujumla ili kukabiliana na changamoto za lishe kwa watoto katika umri wa kuanzia ujauzito, kuzaliwa mpaka angalau miaka 2 toka kuzaliwa, ambayo kitaalamu imeelezwa kwamba ni siku elfu moja (1000) za kukabiliana na lishe duni kwa watoto. Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa kikao na Afisa Utumishi wa Wilaya hiyo Bi. Gladness Mwano amewashukuru wajumbe wote na kuwaasa kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake kwa jamii, hususani kundi lengwa la watoto wadogo ili kuikoa jamii na madhara yatokanayo na lishe duni katika Wilaya yetu
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.