DHANA YA MTAKUWWA
Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kupitia Mendeleo ya Jamii tunaendelea kutoa elimu na kupinga vikali juu ya masuala mbalimbali yanayo chochea Ukali wa Kijinsia ikiwemo,Ukatili kwa Watoto,Ukatili Kwa Wanawake lakini pia Ukatili kwa Wanaume pamoja na utoaji wa elimu na uhamasishaji wa lishe bora.
MTAKUWWA ni Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Serikali ilianziasha Mpango huu miaka mitano, kuanzia 2017/2018 hadi 2021/22,ikiwa na lengo la kuhakikisha kuwa, jamii inaepukana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, lakini pia inakuwa chachu ya kuwa mabalozi wa kuhakikisha ulinzi na usalama wa wanawake na watoto unazingatiwa katika nyanja mbalimbali.
MAENEO MAKUU MANANE YA KUZINGATIA ILI KUPAMBANA NA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO
Mila na Desturi
Mazingira Salama
Malezi, kuimarisha mahusiano na kuziwezesha familia
Utekelezaji na usimamizi wa sheria
Utoaji huduma kwa waathirika wa ukatili
Mazingira salama shuleni na stadi za maisha
Uratibu, Ufuatiliaji na Tathimini
Haki tano muhimu za mtoto
Haki ya Kuishi. Hii inaanza pale mama anapopata ujauzito. Kukua vizuri kwa mimba kunategemea afya, lishe na mazingira anamoishi mama. Pia kuishi kwa mtoto baada ya kuzaliwa kunategemea upatikanaji wa mahitaji ya msingi, ambayo ni chakula cha kutosha na chenye ubora unaotakiwa, huduma bora za afya na ulinzi toka kwa wazazi, jamii na Serikali. Vifo vya watoto wadogo hutokana na ukosefu wa moja ya mahitaji tajwa hapo juu.
Haki ya Kuendelezwa. Kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania, maendeleo ya mtoto yanahusiana na mtoto kuwa na kiwango kinachokidhi makuzi kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili na kijamii. Ili mtoto aweze kukua vizuri anahitaji kutunzwa, kuongozwa na kulelewa katika misingi mizuri. Mathalani, kuendelezwa kwa mtoto kimwili ni kukua kimaumbile na uzito kwa uwiano wa umri. Hali hii inategemea lishe na huduma bora za afya ikiwemo kupatiwa chanjo zote muhimu na upatikanaji wa viinilishe vyote muhimu. Maendeleo ya mtoto yanahitaji jitihada toka kwa mzazi, jamii na Serikali kwa pamoja.
Haki ya Kulindwa. Inahusu kuzuia vitendo viovu wanavyofanyiwa watoto katika hatua za ukuaji wao, kabla na baada ya kuzaliwa. Mathalani, mtoto anahitaji ulinzi dhidi ya kazi nzito zisizowiana na umri wake, kudhulumiwa mali hasa kwa watoto yatima, kutupwa au kutelekezwa na wazazi, utoaji mimba wa makusudi, kuonewa nk. Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania pia inasisitiza juu ya ulinzi dhidi ya unyanyasaji wa mtoto ikiwemo kukeketwa, kulazimisha kuolewa/kuoa katika umri mdogo, ubakaji, nk.
Haki ya Kushiriki.
Ushiriki wa mtoto unapatikana pale mtoto anapopewa nafasi kikamilifu katika kutoa mawazo, kushiriki katika maamuzi ya masuala yanayohusu maendeleo yake, nk. katika hatua mbalimbali za ukuaji wake. Kitaalamu hatua za ushiriki wa mtoto huanza rasmi kuanzia umri wa miaka mitatu hadi anapokuwa mtu mzima. Misingi ya ushiriki wa mtoto huzingatia umri na aina ya masuala anayopaswa kushirikishwa.
Haki ya Kutobaguliwa. Ubaguzi wa mtoto umegawanyika katika makundi mbalimbali, katika yote yapo makundi makuu mawili. Ubaguzi wa kijinsia ambao mtoto wa kike au wa kiume anaweza kubaguliwa na wazazi, walezi au jamii. Upo ubaguzi unaotokana na hali yake ya kimaisha kama vile utajiri au umasikini, ulemavu, ugonjwa, uyatima na jinsi anavyoonekana mbele za watu. Mfano wa kuumiza ni ubaguzi wa kimfumo ambapo hapa kwetu takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia moja tu ya watoto wenye ulemavu wanaondikishwa kujiunga na elimu ya msingi. Hii inaathiriwa na mtazamo wa kijamii dhidi ya watoto hawa kwani wazai huwafungia ndani ili kuficha aibuhivyo kuwanyima fursa ya kupata elimu.
MALEZI, MSAADA NA UHUSIANO KATIKA FAMILIA
MALEZI
Malezi ni utoaji wa huduma muhimu kwa mtoto zikiwemo lishe, ulinzi, afya,elimu na uchangamshi.
Ni kumkinga mtoto na aina zote za ukatili na kumpa haki stahiki za kuishi, kuendelezwa,ulinzi,kushiriki na kutobaguliwa
Ni mchakato wa kumwendeleza mtoto kufikia malengo yake anapokuwa mtu mzima
Huduma muhimu za malezi
Mtoto anahitaji huduma mbalimbali za afya ili aweze kukua kulingana na umri wake
Kabla ya mtoto kuzaliwa mama anahitajika kuhudhuria kliniki ili apate chanjo na kinga nyingine za maradhi kudhibiti ukuaji wa mtoto
Baada ya kuzaliwa mtoto anahitaji chanjo nyingine kama kifua kikuu na polio na baadae kichomi, kifadulo, pepopunda, donda koo, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo, kukinga kuharisha na surua
Chanjo hizi humkinga mtoto na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kuhatarisha maisha yake.
Mtoto anahitaji lishe bora na anatakiwa kunyonya maziwa ya mama katika kipindi cha miezi sita (au itakavyoshauariwa vinginevyo) ili apate viinilishe muhimu kutoka kwa mama.
Lishe bora inamwepusha mtoto na magonjwa, utapiamlo na kusababisha mtoto kuwa na uzito mdogo na hatimaye kuzorotesha ukuaji wake.
Madini mbalimbali kwenye chakula mf. Madini joto humfanya mtoto azalishe damu mwilini na kuimarisha mifupa hivyo ubora wa chakula cha mtoto ni muhimu kudhibitiwa.
Ulinzi wa mtoto – Kumlinda mtoto dhidi ya aina zote za ukatili ikiwemo ukatili wa kimwili, kiakili na kisaikolojia.
Aina za ulinzi wa mtoto
Ulinzi ambao mzazi/mlezi anautoa kwa mtoto
Uwezo anaojengewa mtoto katika kujilinda mfano kuwa na maadili na kuepuka tabia zenye madhara.
Ulinzi ambao unawekwa na mfumo (Serikali, mahakama na au Bunge) kulinda mtoto, familia na jamii kwa ujumla mfano sheria, taratibu na kanuni.
Elimu ni muhimu katika kumuendeleza mtoto ili aweze kupata ufahamu, ujuzi na uelewa wa kuweza kumudu mazingira yake na kujenga mahusiano mazuri kati yake na jamii.
Kuna aina mbili za elimu ambazo ni elimu rasmi mf. Shule, chuo n.k. na elimu isiyo rasmi, ambayo hutolewa kwa mtoto na wazazi na wanajamii kutokana na uzoefu wa mazingira au aina ya matukio yafananayo ili kumsaidia mtoto kumudu hali au mazingira yanayomkabili. Mf Maonyo, Makaripio, Jando, Unyago, dini, au hata wosia.
Maadili ya mtoto yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mchanganyiko wa upatikanaji wa huduma za elimu na malezi katika jamii
Uchangamshi wa awali wa mtoto ni huduma anazopewa mtoto kwa lengo la kumjenga kiakili na kimwili ili aweze kukabiliana na mazingira yake.
Huduma hii uhusisha michezo, vitendo vya upendo kutoka kwa jamii, matumizi ya vifaa vya kuburudisha nk.
Huduma hii ni muhimu katika kujenga saikolojia na utimamu wa mtoto.
UHUSIANO KATIKA FAMILIA
Mahusiano katika familia husaidia kujenga mazingira yanayotoa fursa ya mazungumzo katika familia kwa kuhususisha wazazi/walezi na ndugu wengine katika familia.
Watoto wanapaswa kushiriki katika masuala mbalimbali ya familia kulingana na uwezo wao wa kutoa mawazo.
Mazingira mazuri yatapunguza matukio ya tabia hatarishi na kuongeza matukio ya tabia inayokubalika.
Wanafamilia wote katika kaya wanapaswa kushiriki katika ukuaji wa watoto kimwili na kiakili.
Uhusiano kati ya malezi ya watoto na mahusiano ya wazazi/walezi kwenye familia ni hatua mojawapo ya msingi katika kumuwezesha mtoto kuishi katika mazingira salama.
UKATILI WA KIJINSIA
Ni kitendo chochote anachofanyiwa mtu kutokana na jinsi yake au majukumu yake ya kijinsia. Kitendo hicho ni kile ambacho kinaweza kumuathiri mtu kimwili, kiakili, kijinsia au kisaikolojia.
Ukatili wa kijinsia una madhara zaidi kwa wasichana na wanawake kuliko wanaume na wavulana. Aidha, aina na ukubwa wa ukatili unatofautiana kati ya mikoa na mikoa, tamaduni na tamaduni.
2.1 UKATILI WA KIMWILI: Ni kitendo anachofanyiwa mtu kinachohusisha kuumizwa mwili na huweza kuonekana moja kwa moja au mwathirika kuhisi maumivu bila watu wengine kutambua kitendo hicho.
Mifano ya ukatili wa kimwili ni vipigo, shambulio la mwili, kuchomwa mwili na moto au ncha kali, matumizi ya silaha, kuvuta nywele, kusukuma au ukatili wowote mwingine.
2.2 UKATILI WA KISAIKOLOJIA/ KIHISIA: Ni ukatili ambao mtu anatendewa na unamsababishia maumivu kiakili/kihisia ambapo mtu mwingine hawezi kutambua kuwa mwenzake ametendewa utakili hadi mazingira yatakapojitokeza na mtendewa akajieleza.
Mifano ya ukatili wa kihisia/kisaikolojia ni matusi kwa njia ya maneno au ishara yenye lengo la kudhalilisha, vitisho na kutishia kufanya fujo, maneno ya kufedhehesha, kudharauliwa hadharani, kutishia kutoa siri, kuingiliwa faragha, kutishiwa kuuawa, wivu wa kupindukia,kunyang’anywa watoto kwa makusudi n.k. Ukatili wa kimwili una madhara mengi kama vile majeraha, ulemavu na wakati mwingine hupelekea hadi kifo.
2.3 UKATILI KATIKA UHUSIANO WA KINGONO: Ukatili huu huambatana vitendo vinavyohusiana na masuala ya ngono. Mfano unyanyasaji/bugudha za kjinsia, kujaamiana kwa maharimu, ubakaji ndani ya ndoa, ulawiti, utekaji na usafirishaji wa wanaume au wanawake na watoto kwa ajili ya ngono, utumwa wa kingono, mashambulio na kuingiza vitu vigumu kwenye sehemu za siri. Madhara yanayotokana na aina hii ya ukatili ni pamoja na uharibifu wa mfumo wa uzazi pindi mtoto anapofanyiwa kitendo cha ubakaji. Magonjwa kama vile UKIMWI, Mimba za utotoni nk.
2.4 UKATILI WA KIUCHUMI: Ni aina ya ukatili ambao unamnyima fursa za kiuchumi mwanamke au mwanaume katika kujiongezea kipato na kuchangia katika maendeleo. mfano wa ukatili huu ni kunyang’anywa mali, ubaguzi katika fursa za kiuchumi na umiliki wa mali, kukosa fursa za kujielimisha na vinginevyo.
2.5 UKATILI UNAOTOKANA NA TAMADUNI AU MILA POTOFU: Huu unatokana na mila na desturi za jamii zetu ambazo zinaenda kinyume na haki za binadamu hivyo kuchangia kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia. Kwa mfano, ndoa za kushurutisha, ndoa za utotoni, kutakasa wajane, ukeketaji, ndoa za maharimu, kuwekwa ndani kwa shuruti, miiko ya chakula na ukatili utokanao na mahari.
3.0 Maeneo ambayo ukatili wa Kijinsia hujitokeza kwa kiwango kikubwa
Familia: Ni moja ya sehemu ambayo nguvu iliyopo katika kaya au familia inasababisha ukatili wa kijinsia kwa kuwa ukatili katika familia na kaya hutokea majumbani na mara nyingi huonekana kama ni suala la binafsi na kufanya upatikanaji wake wa taarifa kuwa mgumu.
Jumuiya/jamii: Kwa kukubaliana na tabia au mwenendo wa wanaume wanaofanya ukatili unaolenga katika kuwamiliki wanawake, jumuiya au jamii inakuwa ni kitovu cha ukatili wa kijinsia.
Katika mitandao ya kijamii: katika mitandao ya kijamii hususani katika simu janja, picha zinazovunja heshima ya mtu zimekuwa zikisambazwa, zikiwemo picha za ngono.
Katika taasisi mbalimbali: Maeneo hayo yamekuwa ni sehemu ambayo ukatili wa kijinsia hufanyika kwa kiwango kikubwa, hasa pale mwanamke anapohitaji huduma mbalimbali. Katika maeneo hayo, wanawake hupapaswa maungo yao, hubakwa, hukejeliwa na kufanyiwa vitendo kama hivyo.
4.0 Sababu zinazopelekea Ukatili wa Kijinsia
Mila na Desturi Potofu-Mila na Desturi huchangia katika aina zote za ukatili wa kijinsia.
Baadhi ya Mila na Desturi ambazo zimekuwepo tangu zamani zimekuwa zikichochea sana suala la ukatili wa kijinsia, kwani humfanya mwanamke kuwa mnyenyekevu na kushindwa hata kudai haki zake. Baadhi ya maeneo, kumpiga mwanamke imekuwa ni utamaduni, lakini katika mazingira ya kawaida ya maisha, hata kumsaidia mwanamke kazi za ndani inatasfiriwa vibaya, lakini pia wanawake wanazuiwa hata kumiliki mali za familia. Lakini baadhi ya mila zinaona kuwa, kumpiga mwanamke ni njia sahihi ya kumuadhibu.
Umasikini - ambapo watoto wa kike na kwa baadhi ya maeneo wa kiume hutumikishwa katika majukumu yaliyo juu ya uwezo wao ili waweze kumudu gharama za maisha. Mifano ni kuajiri wadada wa kazi walio chini ya umri unaostahili, kutumikisha watoto wadogo katika shughuli hatarishi kama migodi, ziwani na kumbi za starehe. Aidha, uhaba wa rasilimali zinazotusaidia kuishi zinawaweka katika hatari wanawake na wasichana, lakini vilevile kuhangaika kuzipata ili kuhakikisha maisha ya wanafamilia wengine yanaendelea. Hali hii wakati mwingine huwaweka hata katika hatari ya kubakwa.
Matumizi ya pombe na madawa ya kulevya: ambapo baada ya kutumia vilevi, watendaji wa matukio hayo hukosa maamuzi yenye busara na kufanya vitendo mbalimbali vya ukatili ikiwemo kupiga wenza, kulazimisha ngono, kutukana na kulazimisha mke kufanya majukumu mengine kinyume na utashi wake.
Sababu nyingine ni kama vile:
-Kukithiri kwa mfumo dume ambao unawapendelea wanaume na kutoa nafasi kidogo kwa wanawake kwenye maamuzi, kumiliki rasilimali na majukumu ya kazi.
-Tafsiri potofu ya maandiko ya vitabu vya dini:
- Kupokea mahari bila ridhaa ya mwanamke
- Ufahamu mdogo wa haki za binadamu
5.0 Changamoto inayosababisha kuendelea kwa hali za ukatili wa kijinsia
-Wahanga wa ukatili wa kijinsia kushindwa kutoa taarifa katika mamlaka za juu
Ukatili wa kijinsia kwa sehemu kubwa unafanywa na watu walio karibu. Hivyo, wahanga kutoa taarifa kunasababisha watendaji wa uovu kupelekwa katika vyombo vya kisheria. Hivyo, ili kumlinda ndugu huyo wa karibu, wahanga hawatoi taarifa ya vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa.
Vitendo vya ukatili kuwa kama sehemu ya mila na desturi, hivyo kuvizuia ni sawa na kuzuia mila na desturi hizo.
Kushindwa kufahamu haki na wajibu wa wahanga baada ya kufanyiwa vitendo vya ukatili.
6.0 Nini kifanyike:
Chukua hatua na vunja ukimya: Wasaidie wahanga wa Ukatili wa Kijinsia kuepuka manyanyaso katika jamii na kupatiwa huduma za msaada wa kisheria, kisaikolojia na hata matibabu ya afya.
-Kuendelea kutoa elimu za masuala ya jinsia katika namna mbalimbali
-Toa taarifa kwa vyombo vya dola, Serikali na hata asasi za kiraia pindi unapofanyiwa au kushuhudia vitendo vya Ukatili wa Kijinsia kwa msaada zaidi wa kisheria.
--Kuimarisha wanawake kiuchumi kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kupitia vikundi, na pia kuziwezesha kaya zenye kipato duni kuwa na kipato endelevu kupitia mpango wa TASAF.
-Kuendelea kuhamasisha wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kutoa uwanja mpana wa kujadili changamoto wanazokutana nazo.
- Kuendelea kufanya maazimisho ya siku zote muhimu za kitaifa, ikiwemo siku ya Sheria, Siku ya Wanawake, siku ya Mtoto, siku16 za kupinga ukatili wa kijinsia (kuanzia tarehe (25/11 hadi 10/12 ya kila mwaka) ili kujenga uelewa zaidi ya masuala ya jinsia.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.