Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Antony Mtaka amesema Wilaya ya Makete itakuwa ya mfano katika mkoa kwa uzalishaji wa zao la ngano.
Akizungumza leo 16 Septemba 2022 kwenye Mkutano wa wadau wa zao la ngano uliofanyika ukumbi wa Madihani Villa Makete Mjini, Mhe. Mtaka amesema kutokana na uhitaji mkubwa wa zao hilo nchini Wilaya ya Makete inatarajia kuzalisha kwa wingi katika maeneo mengi wilayani hapa.
Pia Mhe. Mtaka amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda, Mkurugenzi Mtendaji Wilaya William Makufwe na watumishi kwa uthubutu katika kuwaza namna ya kuwa na zao la kimkakati katika uzalishaji wa Ngano Wilayani Makete.
“Nawapongeza sana Viongozi wa Halmashauri kwa kufikiri nje ya boksi katika kuona njia rahisi ya kuwakwamua wananchi kiuchumi mnamsaidia Mhe. Rais vizuri katika kutekeleza majukumu ya kimsingi kwa wananchi”.
“Wilaya ya Makete hakuna mtu masikini zaidi niwasisitize watu walime ngano kwa wingi tuachane na suala la kuzungumzia umasikini Makete kwa kuwa ardhi iliyopo inautajiri wakutosha na karibu mazao mengi yanastawi vizuri hasa ngano”
Pia Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza kuitishwa mkutano wa wenyeviti wa Vijiji kutoka vijiji vyote vinavyozalisha ngano mwishoni mwa mwezi huu ili kukubaliana namna ya kuanza uzalishaji wa ngano mapema mwakani katika maeneo yote yanayopaswa kulima ngano.
Wakati huohuo amewaagiza maafisa Kilimo kuainisha majina ya wakulima, kiasi cha mashamba na idadi ya mashamba wanayotaka kulima ngano ili kurahisisha ongezeko la uhamasishaji wa kilimo cha zao hilo.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mkurugenzi wa Bodi ya mazao mchanganyiko Dkt. Anselm Moshi, wakurugenzi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Njombe, waheshimiwa wenyeviti wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya, waheshimiwa Madiwani Wilaya ya Makete, Taasisi ya kifedha, Maafisa Kilimo, wadau wa Kilimo na wakulima kutoka vijiji zaidi ya 90 vya Wilaya ya Makete
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.