Ludewa — Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Mhe. Wise Mgina, amepongeza jitihada za Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa kutoa motisha kwa shule zilizopata matokeo bora katika mitihani ya kidato cha tano na cha sita. Pongezi hizo alizitoa wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo uliofanyika jana, ambapo aliwapongeza viongozi na walimu kwa kujituma kuboresha elimu katika wilaya hiyo.
Mhe. Mgina alieleza kuwa hatua ya kutoa motisha kwa shule zilizofaulisha kwa viwango vya juu ni ya kupongezwa, kwani inachochea ari ya kujifunza kwa wanafunzi na kuimarisha jitihada za walimu katika kufundisha. Alisisitiza kuwa motisha hiyo inachangia kuhamasisha shule zingine kuhakikisha zinafanya vizuri zaidi katika mitihani ijayo.
"Napenda kumpongeza Mkurugenzi wetu kwa kutoa motisha kwa shule zilizofanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha tano na sita. Hii ni hatua muhimu inayothibitisha jinsi tunavyojikita kuinua viwango vya elimu katika wilaya yetu. Tunataka kuona mafanikio haya yanakua na kuhamasisha shule nyingine kufikia viwango vya juu zaidi," alisema Mhe. Mgina.
Aidha, aliwataka walimu na wanafunzi kuendelea kujituma na kuweka juhudi zaidi ili kuhakikisha wanapata matokeo bora zaidi. Alieleza kuwa Halmashauri itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu kwa lengo la kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kujengea uwezo wa walimu.
"Natoa wito kwa walimu na wanafunzi kuendelea kujituma. Serikali yetu ipo bega kwa bega na nyie, na tutahakikisha tunaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Motisha hii ni mwanzo tu wa jitihada endelevu," aliongeza.
Katika hotuba yake, Mhe. Mgina aliwahimiza viongozi wa shule na jamii kwa ujumla kuunga mkono mipango ya kuboresha elimu na kuwekeza zaidi katika sekta hiyo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na kujiandaa vyema kwa maisha ya baadaye.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.