MRADI NA. 5441-TCRP, MKURUGENZI AKABIDHI VYUMBA VYA MADARASA CHIEF KIDULILE SEKONDARI; UKAMILISHAJI MAENEO MENGINE UNAENDELEA KWA KASI
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Bwana Sunday Deogratias amemkabidhi Mheshimiwa Andrea Tsere, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari Chief Kidulile. Katika Hafla fupi iliyofanyika Shuleni hapo, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa amemshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa fedha kiasi cha Tsh. 940,000,000/= (Mia Tisa Arobaini Milioni) ambazo zimewezesha ujenzi wa Vyumba vya madarasa 47 katika Shule zote 17 za Sekondari zilizipo katika Halmashauri hiyo.
Katika Picha, Mheshimiwa Andrea Tsere (watatu kutoka kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Ludewa akiwa katika picha ya Pamoja na Mheshimiwa Monica Mchilo (kulia kwake) na Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Sunday Deogratias na wajumbe wa kamati ya Ujenzi ya Chief Kidulile baada ya makabidhiano ya vyumba vinne vya madarasa.
Aidha amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha anawasimamia watendaji na uongozi katika Shule hiyo kuhakikisha wanalinda miundombinu yote ya mradi huu kwani Serikali Inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haitakubali kuona mradi unaharibiwa mapema kabla hata ya kupata matokeo yaliyokusudiwa. Amemtaka kumuagiza Mkuu wa Shule hiyo kuweka alama maalumu katika viti na meza za wanafunzi kabla ya kuwagawia, na wahakikishe wanawapa elimu ya kutunza samani hizo na majengo.
Katika habari picha ni viti na meza vikiwa vimepangwa katika moja ya vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari Chief Kidulile.
Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata ya Ludewa Bi. Monica Mchilo ameishukuru Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi, chini ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Kata yake ya Ludewa katika Shule hiyo Kiasi cha Tsh. Milioni themanini (80,000,000/=) zilizowezesha kukamilisha ujenzi wa madarasa manne, na hiyo itapelekea kuepusha msongamano wa wanafunzi pindi shule zitakapofunguliwa. Amemhakikishia Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Ludewa kwamba yeye na wananchi waliomchagua wa Kata ya Ludewa wanamuunga Mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi kubwa anazofanya kuliletea maendeleo Taifa, ikiwemo Wilaya ya Ludewa ambayo imepatiwa fedha nyingi sana katika miradi mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji akitoa salam za shukrani kwa niaba ya uongozi na watendaji wa Halmashauri, Amemshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa fedha alizoipatia Halmashauri ya Ludewa katika Mradi huu (Mradi Na. 5441- TCRP), katika sekta ya Afya, Elimu, na amemhakikishia Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kwamba maagizo yote aliyoyatoa yatazingatiwa na kwamba atahimiza juhudi kubwa ziendelee katika kukamilisha mradi huu katika maeneo mengine, hususani Kata ya Makonde katika Sekondari ya Makonde kwani inakabiliwa na changamoto kubwa ya usafirishaji vifaa kupitia Ziwa Nyasa. Hata hivyo ameendelea kuwatia moyo wakazi wa Kata ya Makonde kwani licha ya changamoto hiyo, wamefikia hatua nzuri sana na atahakikisha anawasimamia wakamilishe kwa wakati ujenzi wa madarasa katika Shule iliyopo katika kata hiyo.
Sehemu ya ndani ya moja ya madarasa ya Shule ya Sekondari Chief Kidulile, katika Mradi Na. 5441-TCRP. Taa zikiwa zinawaka na viti na meza vimepangwa kwa unadhifu mkubwa, ikiwa ni ishara ya kukamilika kwa mradi katika Shule hii. Kazi Iendeleee.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Ndugu Sunday Deogratias, akitoa salam za Shukrani mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ludewa (aliyeketi mbele kabisa kushoto) katika hafla ya makabidhiano ya vyumba vinne vya madarasa Shuleni Chief Kidulile Sekondari.
Diwani wa Kata ya Ludewa (CCM) Bi. Monica Mchilo akiteta jambo na Mheshimiwa Andrea Tsere, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa katika hafla ya makabidhiano ya vyumba vinne vya madarasa ya Mradi Na.5441-TCRP. Wengine katika msitari wa mbele ni Ndugu Sunday Deogratias, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa (watatu kutoka kushoto) na Ndugu Onesmo V. Haule, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Chief Kidulile.
Vyumba vinne vya madarasa katika Mradi Na.5441-TCRP katika Shule ya Sekondari Chief Kidulile baada ya kukamilika ujenzi wake na kukabidhiwa kupitia Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Ludewa.
Madarasa ya Mradi Na.5441-TCRP muonekano wa upande wa nyuma baada ya kukamilika katika Shule ya Sekondari Chief Kidulile tarehe 23-12-2021.
Kwanza tupambe, kishaaaa tusherehekeeeee. Ndicho unachoweza kusema, baada ya Shughuli pevu, wananchi wa kata ya Ludewa, wakiongozwa na Mheshimiwa Monica Mchilo Diwani wao, wanafurahia kukamilika kwa Mradi Na.5441-TCRP, vyumba vinne vya madarasa vilivyogharimu Tsh. 80,000,000/= zilizotolewa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Shule ya Sekondari Chief Kidulile iliyopo katika kata ya Ludewa. Katika habari picha, Mheshimiwa Andrea Tsere na wadau mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja baada ya makabidhiano.
Ni furaha na vicheko tu baada ya kumalisha ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari Chief Kidulile.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.