Mbunge wa Jimbo la Ludewa Mkoani Njombe Mhe. Deo Ngalawa amewaasa wananchi wa Jimbo la Ludewa Kumuunga Mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika juhudi kubwa anazofanya kuliletea Taifa letu Maendeleo.
Akizungumza kwa hisia katika Kikao cha Baraza la Madiwani, Mhe. Ngalawa amesema Nchi hii ilikuwa imefika mahali pabaya sana kiasi kwamba maskini na wanyonge walikuwa hawana haki katika Taifa hili. Hivyo wakati Mheshimiwa Rais akifanya juhudi za makusudi kuleta usawa baina ya wananchi yapaswa kumuunga mkono juhudi zake kwa gharama zote na kwa moyo wote.
"Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu amedhibiti mianya yote ya Rushwa, amekomesha ufisadi, matokeo yake sasa tunaona miradi mikubwa mingi ikitekelezwa kwa fedha zetu wenyewe" alisema Mheshimiwa Ngalawa. Aliongeza kwa kusema, sasa hivi Mhe. Rais amenunua Ndege nane kwa mpigo, ambapo sita tayari zimewasili nchini, anajenga Reli ya Standard Gauge, anajenga mradi mkubwa wa Umeme Mto Rufiji, Vituo vya Afya, hapa kwetu ametupatia fedha za kujenga na kukarabati vituo vinne na karibia kila kata nchini ujenzi wa vituo vya Afya, maboma ya shule unaendela na pia umekamilika maeneo mengi sana, Hospitali za Wilaya. Ni lazima tujivunie na Tumpongeze Rais wetu kwa juhudi hizi.
Katika Mkutano huo wa Baraza la Madiwani uliofanyika siku ya Jumamosi tarehe 17, Agost 2019 Mheshimiwa Mbunge Ngalawa pia alishauri wananchi kuongeza juhudi katika mapambano dhidi ya rushwa, kukemea ufisadi na kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo. Alitumia Mkutano huu kumshukuru Mhe. Rais kwa Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha zege toka Iton-Ludewa-Manda kipande cha urefu wa kilometa 50 toka Lusitu mpaka Mawengi. Akizungumzia Mradi huu, Mheshimiwa Mbunge Ngalawa amesema kwa Wanaludewa, hii ni heshima kubwa sana kwetu kwani Ujenzi wa aina hii ni wa gharama kubwa sana, na urefu wa km 50 kwa kiwango cha zege ni wa kipekee katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mh. Andrea Tsere amempongeza Mheshimiwa Mbunge Ngalawa kwa kushiriki Mkutano huo wa Baraza la Madiwani. Akitoa salaam za Serikali Kuu, Mhe. Mkuu wa Wilaya amesema kwamba umoja na mshikamano ndio nguzo ya mafanikio ya Ludewa. Alisisitiza kwamba umoja na mshikamano uliopo kati ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Halmashauri yaani Mhe. Mwenyekiti, Madiwani wote, Wataalam na watumishi wote (Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji) wanafanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu sana na hivyo kuleta tija kwa wananchi wa Ludewa na Taifa kwa ujumla.
Amewataka wananchi wote kuhakikisha wanashiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.