Na Chrispin Kalinga
Wizara ya Afya inaendelea kuikinga jamii ya Watanzania dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo ambayo ni Kifua kikuu, Donda Koo, Kifaduro, Polio, Surua, Rubella, Pepo punda, Homa ya ini, Homa ya uti wa mgongo, Kichomi, Kuhara na Saratani ya shingo ya kizazi.
Hayo yote aliyaeleza Mratibu wa Chanjo wa Wilaya ya Ludewa Bw. James Kadege wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya chanjo yaliyofanyika katika kata ya Ludewa tarehe 6 Mei 2023, ikumbukwe kwamba wiki ya chanjo inaongozwa na kauli mbiu isemayo “ Tuwakinge wote Kwa Chanjo ” ikienda sambamba na ujumbe usemao “Jamii Iliyopata Chanjo, Ni Jamii Yenye Afya”.
“Wizara ya Afya iliweka huduma ya Chanjo kuwa kipaumbele cha kwanza kati ya vipaumbele vyake kumi kwa mwaka 2022/2023. Katika kufikia malengo ya kipaumbele hiki, Wizara imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja huduma tembezi za mkoba ili kuhakikisha walengwa wote wanapata Chanjo”.alieleza Bw. Kadege
Maadhimisho ya Wiki ya Chanjo Kiwilaya yalifanyika katika viwanja vya Zahanati ya kijiji cha Ludewa kijijini na Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mhe. Victoria Mwanziva akiwakilishwa na Bw. Linus Malamba, katika hotuba yake aliwahimiza Wazazi na walezi kutumia wiki ya chanjo kuwapeleka watoto wote ambao hawajapata chanjo na ambao hawajamaliza ratiba ya chanjo kwenye Vituo vya Kutoa Huduma za Afya ili waweze kupatiwa chanjo bila gharama yoyote.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.