Hatimaye wananchi wa tarafa ya Liganga Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wameondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya afya waliyokuwa wakikabiliana nayo hapo awali baada ya ujenzi wa kituo cha afya kilichokuwa kikijengwa katika kata ya Mundindi kukamilika kwa asilimia 99.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo hicho mwenyekiti wa kamati ya ujenzi Bwana. Benedict Mhagama katika uzinduzi wa uanzishwaji huduma kituoni hapo amesema hatua hiyo ya ujenzi imefikiwa kwa michango ya wananchi, mbunge, halmashauri kwa kiasi cha sh. Ml. 89 huku serikali kuu ikitoa fedha za tozo kiasi cha sh. Ml. 500.
“Awamu ya kwanza Rais Samia alituletea kiasi cha sh. Ml. 250 ambazo zilitumika kwa ujenzi wa jengo la OPD, Maabara, kichomea taka, nyumba ya watumishi ambapo majengo yote hayo kwa sasa yamekamilika kwa asilimia 99 na awamu ya pili alituletea Ml. 250 nyingine kwaajili ya jengo la huduma ya mama na watoto, upasuaji, pamoja na jengo la kufulia ambayo kwasasa yamefikia hatua ya kuezeka”. Amesema Mhagama.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri Wise Mgina ambaye pia ni diwani wa kata hiyo amemshuku Rais Samia kwa kuwapa fedha za kukamilisha ujenzi huo huku akiwataka watanzania kuacha kulalamikia tozo za simu kwakuwa ndizo zinazoleta maendeleo katika huduma za msingi.
“Mwanzoni tozo zilipoanza watu walikuwa wakilalamika sana, lakini kwa sasa natumai walio wengi wameelewa faida ya tozo” Amesema Wise.
Gerald Usili ni katibu tarafa ya Mawengi, akimuwakilisha mkuu wa wilaya ya Ludewa ameishukuru serikali kuu na kuwataka wauguzi kufanya kazi kwa weledi na kufuata miongozo yao ya kazi.
Amesema Ofisi ya mkurugenzi kupitia mganga mkuu inapaswa kuendelea kutuma maombi ya fedha serikali kuu kwajili ya kuongezeza majengo mengine ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya wagonjwa kama huduma za mionzi, macho, Pharmacy, vyumba vya waganga, wodi za wagonjwa pamoja na mochwari.
Aidha kwa upande wake mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Stanley Mlay amesema kwa sasa kituo hicho kitakuwa na watumishi kumi na sita ambapo wataendelea kuongezeka kulingana na kukua kwa huduma.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kujenga mazoea ya kupata vipimo pindi wanapohisi kuumwa badala ya kunywa dawa pasipo kujua tatizo la ugonjwa wake.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.