UKATILI WA KIJINSIA
Ni kitendo chochote anachofanyiwa mtu kutokana na jinsi yake au majukumu yake ya kijinsia. Kitendo hicho ni kile ambacho kinaweza kumuathiri mtu kimwili, kiakili, kijinsia au kisaikolojia.
Ukatili wa kijinsia una madhara zaidi kwa wasichana na wanawake kuliko wanaume na wavulana. Aidha, aina na ukubwa wa ukatili unatofautiana kati ya mikoa na mikoa, tamaduni na tamaduni.
2.1 UKATILI WA KIMWILI: Ni kitendo anachofanyiwa mtu kinachohusisha kuumizwa mwili na huweza kuonekana moja kwa moja au mwathirika kuhisi maumivu bila watu wengine kutambua kitendo hicho.
Mifano ya ukatili wa kimwili ni vipigo, shambulio la mwili, kuchomwa mwili na moto au ncha kali, matumizi ya silaha, kuvuta nywele, kusukuma au ukatili wowote mwingine.
2.2 UKATILI WA KISAIKOLOJIA/ KIHISIA: Ni ukatili ambao mtu anatendewa na unamsababishia maumivu kiakili/kihisia ambapo mtu mwingine hawezi kutambua kuwa mwenzake ametendewa utakili hadi mazingira yatakapojitokeza na mtendewa akajieleza.
Mifano ya ukatili wa kihisia/kisaikolojia ni matusi kwa njia ya maneno au ishara yenye lengo la kudhalilisha, vitisho na kutishia kufanya fujo, maneno ya kufedhehesha, kudharauliwa hadharani, kutishia kutoa siri, kuingiliwa faragha, kutishiwa kuuawa, wivu wa kupindukia,kunyang’anywa watoto kwa makusudi n.k. Ukatili wa kimwili una madhara mengi kama vile majeraha, ulemavu na wakati mwingine hupelekea hadi kifo.
2.3 UKATILI KATIKA UHUSIANO WA KINGONO: Ukatili huu huambatana vitendo vinavyohusiana na masuala ya ngono. Mfano unyanyasaji/bugudha za kjinsia, kujaamiana kwa maharimu, ubakaji ndani ya ndoa, ulawiti, utekaji na usafirishaji wa wanaume au wanawake na watoto kwa ajili ya ngono, utumwa wa kingono, mashambulio na kuingiza vitu vigumu kwenye sehemu za siri. Madhara yanayotokana na aina hii ya ukatili ni pamoja na uharibifu wa mfumo wa uzazi pindi mtoto anapofanyiwa kitendo cha ubakaji. Magonjwa kama vile UKIMWI, Mimba za utotoni nk.
2.4 UKATILI WA KIUCHUMI: Ni aina ya ukatili ambao unamnyima fursa za kiuchumi mwanamke au mwanaume katika kujiongezea kipato na kuchangia katika maendeleo. mfano wa ukatili huu ni kunyang’anywa mali, ubaguzi katika fursa za kiuchumi na umiliki wa mali, kukosa fursa za kujielimisha na vinginevyo.
2.5 UKATILI UNAOTOKANA NA TAMADUNI AU MILA POTOFU: Huu unatokana na mila na desturi za jamii zetu ambazo zinaenda kinyume na haki za binadamu hivyo kuchangia kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia. Kwa mfano, ndoa za kushurutisha, ndoa za utotoni, kutakasa wajane, ukeketaji, ndoa za maharimu, kuwekwa ndani kwa shuruti, miiko ya chakula na ukatili utokanao na mahari.
3.0 Maeneo ambayo ukatili wa Kijinsia hujitokeza kwa kiwango kikubwa
Familia: Ni moja ya sehemu ambayo nguvu iliyopo katika kaya au familia inasababisha ukatili wa kijinsia kwa kuwa ukatili katika familia na kaya hutokea majumbani na mara nyingi huonekana kama ni suala la binafsi na kufanya upatikanaji wake wa taarifa kuwa mgumu.
Jumuiya/jamii: Kwa kukubaliana na tabia au mwenendo wa wanaume wanaofanya ukatili unaolenga katika kuwamiliki wanawake, jumuiya au jamii inakuwa ni kitovu cha ukatili wa kijinsia.
Katika mitandao ya kijamii: katika mitandao ya kijamii hususani katika simu janja, picha zinazovunja heshima ya mtu zimekuwa zikisambazwa, zikiwemo picha za ngono.
Katika taasisi mbalimbali: Maeneo hayo yamekuwa ni sehemu ambayo ukatili wa kijinsia hufanyika kwa kiwango kikubwa, hasa pale mwanamke anapohitaji huduma mbalimbali. Katika maeneo hayo, wanawake hupapaswa maungo yao, hubakwa, hukejeliwa na kufanyiwa vitendo kama hivyo.
4.0 Sababu zinazopelekea Ukatili wa Kijinsia
Mila na Desturi Potofu-Mila na Desturi huchangia katika aina zote za ukatili wa kijinsia.
Baadhi ya Mila na Desturi ambazo zimekuwepo tangu zamani zimekuwa zikichochea sana suala la ukatili wa kijinsia, kwani humfanya mwanamke kuwa mnyenyekevu na kushindwa hata kudai haki zake. Baadhi ya maeneo, kumpiga mwanamke imekuwa ni utamaduni, lakini katika mazingira ya kawaida ya maisha, hata kumsaidia mwanamke kazi za ndani inatasfiriwa vibaya, lakini pia wanawake wanazuiwa hata kumiliki mali za familia. Lakini baadhi ya mila zinaona kuwa, kumpiga mwanamke ni njia sahihi ya kumuadhibu.
Umasikini - ambapo watoto wa kike na kwa baadhi ya maeneo wa kiume hutumikishwa katika majukumu yaliyo juu ya uwezo wao ili waweze kumudu gharama za maisha. Mifano ni kuajiri wadada wa kazi walio chini ya umri unaostahili, kutumikisha watoto wadogo katika shughuli hatarishi kama migodi, ziwani na kumbi za starehe. Aidha, uhaba wa rasilimali zinazotusaidia kuishi zinawaweka katika hatari wanawake na wasichana, lakini vilevile kuhangaika kuzipata ili kuhakikisha maisha ya wanafamilia wengine yanaendelea. Hali hii wakati mwingine huwaweka hata katika hatari ya kubakwa.
Matumizi ya pombe na madawa ya kulevya: ambapo baada ya kutumia vilevi, watendaji wa matukio hayo hukosa maamuzi yenye busara na kufanya vitendo mbalimbali vya ukatili ikiwemo kupiga wenza, kulazimisha ngono, kutukana na kulazimisha mke kufanya majukumu mengine kinyume na utashi wake.
Sababu nyingine ni kama vile:
-Kukithiri kwa mfumo dume ambao unawapendelea wanaume na kutoa nafasi kidogo kwa wanawake kwenye maamuzi, kumiliki rasilimali na majukumu ya kazi.
-Tafsiri potofu ya maandiko ya vitabu vya dini:
- Kupokea mahari bila ridhaa ya mwanamke
- Ufahamu mdogo wa haki za binadamu
5.0 Changamoto inayosababisha kuendelea kwa hali za ukatili wa kijinsia
-Wahanga wa ukatili wa kijinsia kushindwa kutoa taarifa katika mamlaka za juu
Ukatili wa kijinsia kwa sehemu kubwa unafanywa na watu walio karibu. Hivyo, wahanga kutoa taarifa kunasababisha watendaji wa uovu kupelekwa katika vyombo vya kisheria. Hivyo, ili kumlinda ndugu huyo wa karibu, wahanga hawatoi taarifa ya vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa.
Vitendo vya ukatili kuwa kama sehemu ya mila na desturi, hivyo kuvizuia ni sawa na kuzuia mila na desturi hizo.
Kushindwa kufahamu haki na wajibu wa wahanga baada ya kufanyiwa vitendo vya ukatili.
6.0 Nini kifanyike:
Chukua hatua na vunja ukimya: Wasaidie wahanga wa Ukatili wa Kijinsia kuepuka manyanyaso katika jamii na kupatiwa huduma za msaada wa kisheria, kisaikolojia na hata matibabu ya afya.
-Kuendelea kutoa elimu za masuala ya jinsia katika namna mbalimbali
-Toa taarifa kwa vyombo vya dola, Serikali na hata asasi za kiraia pindi unapofanyiwa au kushuhudia vitendo vya Ukatili wa Kijinsia kwa msaada zaidi wa kisheria.
--Kuimarisha wanawake kiuchumi kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kupitia vikundi, na pia kuziwezesha kaya zenye kipato duni kuwa na kipato endelevu kupitia mpango wa TASAF.
-Kuendelea kuhamasisha wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kutoa uwanja mpana wa kujadili changamoto wanazokutana nazo.
- Kuendelea kufanya maazimisho ya siku zote muhimu za kitaifa, ikiwemo siku ya Sheria, Siku ya Wanawake, siku ya Mtoto, siku16 za kupinga ukatili wa kijinsia (kuanzia tarehe (25/11 hadi 10/12 ya kila mwaka) ili kujenga uelewa zaidi ya masuala ya jinsia.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.