Ludewa — Shule ya Sekondari ya Chifu Kidulile imepokea zawadi ya shilingi milioni 1.2 kama sehemu ya motisha kwa matokeo bora ya kidato cha sita mwaka huu, zawadi iliyotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ili kuhamasisha juhudi za kuinua kiwango cha elimu. Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mhe. Olivanus Paul Thomas, alitoa pongezi hizo jana katika mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika kujadili maendeleo ya wilaya na mipango ya elimu.
Mhe. Thomas alieleza kuwa zawadi hiyo ni shukrani kwa walimu, wanafunzi, na viongozi wa shule hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya kufikia mafanikio hayo. Alisema kuwa mafanikio ya shule hiyo yanaakisi juhudi za pamoja katika kukuza elimu wilayani Ludewa, na kwamba ni hatua inayopaswa kuigwa na shule nyingine.
"Pongezi za dhati ziwaendee wanafunzi na walimu wa Chifu Kidulile kwa matokeo mazuri waliyopata. Kupitia zawadi hii ya milioni 1.2, tunathibitisha kuwa tunathamini juhudi zinazofanywa kuinua kiwango cha elimu. Tunaamini kuwa hii itachochea ari zaidi kwa shule nyingine katika wilaya yetu," alisema Mhe. Thomas.
Aidha, Mhe. Thomas aliipongeza Halmashauri kwa kuweka mikakati ya kuimarisha elimu na kuongeza ufaulu wilayani humo. Alisema kuwa shule zote wilayani Ludewa zimeonyesha mabadiliko chanya katika matokeo, na akasisitiza kuwa juhudi hizi zinapaswa kuendelezwa kwa kushirikiana na wadau wa elimu.
"Halmashauri yetu imejidhatiti kuhakikisha tunazidi kuongeza ufaulu kwa shule zote. Mafanikio haya yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya walimu, wanafunzi, na jamii kwa ujumla. Tunataka kuona kila shule inafanya vizuri zaidi katika mitihani ijayo," aliongeza.
Mkutano huo wa Baraza la Madiwani ulijadili mipango mbalimbali ya maendeleo wilayani Ludewa, huku suala la elimu likipewa kipaumbele katika kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa bora ya kujifunza na kujiendeleza.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.