Mbunge wa Jimbo la Ludewa Wakili Msomi Mhe. Joseph Zacharius Kamonga amewaasa Waheshimiwa Madiwani Katika Jimbo lake Kujipanga kuipokea miradi mikubwa ya uchimbaji madini ya Makaa ya mawe Mchuchuma na ule wa Chuma Liganga. Akizungumza katika Mkutano cha Baraza la Madiwani. Mhe. Kamonga amesema kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu imedhamiria kuhakikisha miradi hiyo inaanza utekelezaji wake. Amesema kuwa Waheshimiwa Madiwani wahakikishe wanajipanga katika maeneo yao ikiwemo kuona fursa ambazo zinaweza kuwanufaisha wananchi katika maeneo yao wanayoyaongoza. Mheshimiwa Mbunge alitolea mfano, kuanza kuona uwezekano wa kuwaandaa Vijana angalau wawili kutoka maeneo kata wanazoziongoza kuwezeshwa mafunzo ya ujuzi mbalimbali ili itakapofika muda kusikosekane nguvu kazi katika maeneo ya mradi, hali itakayopelekea wawekezaji kutafuta nguvu kazi nje ya maeneo yao, hususani Wilaya ya Ludewa kwa ujumla.
Mheshimiwa Joseph Kamonga (Mb) alitilia mkazo suala hilo kwa kusema kwamba ni lazima kuona namna ya kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kukaa na Wawekezaji kusaidia vijana kupata kozi za ujuzi (fresher course) kama vile udereva kwa vijana kadhaa kutoka kila kata ili kuwa na uwiano wa kunufaika na miradi hii mikubwa Wilaya nzima. Aidha, alisemea pia suala la ujenzi wa Chuo cha VETA katika Kijiji cha Shaurimoyo ambako ndiko uliko mradi wa Chuma-Liganga. Mheshimiwa Mbunge alitumia wasaa huo pia kuwapongeza Waheshimiwa Madiwani wote, Mkurugenzi wa Wilaya na Wataalamu kwa kufanikiwa kukusanya mapato vizuri na kuvuka lengo, ambapo kwa mwaka 2020/2021 Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa imekusanya wastani wa asilimia 112 na hivyo kwa mara ya kwanza kabisa Halmashauri hiyo kukusanya na kuvuka lengo la makusanyo. Halikadhalika amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya kupitia Ofisi ya Biashara kushughulikia kwa haraka madai ya wananchi ya kupanda kwa bei ya mafuta ya kula, kwani kwa maoni yake msimu huu wa mavuno ya mazao mbalimbali ikiwemo Alizeti bei haikupaswa kuwa juu sana mpaka wananchi wawe na malalamiko, pia kuhakikisha wanawatafutia wananchi soko la uhakika la Mahindi kwani ndio zao kuu la biashara na chakula katika Jimbo la Ludewa na Wilaya nzima kwa ujumla.
HABARI PICHA.
Picha 1: Katibu Tawala wa Wilaya ya Ludewa Bi. Zaina Mfaume Mlawa akiwasilisha salam za Serikali Kuu kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya. Kushoto kwake ni Bi Gladness Mwano Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya na katibu wa Mkutano huo wa Baraza la Madiwani akifuatiwa na Mhe. Wise Charles Mgina Mwenyekiti wa Halmashauri.
Picha 2: Baadhi ya Waheshimiwa madiwani wajumbe wa Mkutano wa Baraza, wakiwa katika Mkutano wa robo ya nne na ya mwisho wa mwaka wa fedha wa 2020/2021. Msatari wa mbele kutoka kushoto ni Mhe. Joachim Lukuwi (Iwela), Mhe. Edgar Bosco Mtitu (Lubonde), Mhe. Hamis Kayombo (Mlangali), Mhe. Daniel Thomas Mhagama (Masasi) na Mhe. Rainalda Pius Tweve (Lupingu-Viti Maalum)
Picha 3: Baadhi ya Wananchi wa Ludewa waliohudhuria Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya.
Ludewa - Njombe
Sanduku la Barua: 19
Simu: 026-2790120
Simu ya Rununu:
Barua Pepe: ded@ludewadc.go.tz
Copyright ©2022Ludewadc . All rights reserved.